MBALAMWEZI.
Weye ndiye mbaamwezi, katika usiku wangu,
Laili kwenda siwezi, bila ya wewe mwenzangu,
Fanya hima mkumbazi, liangaze anga langu,
Nakuhitaji mwenzangu, kuishi peke siwezi.

Nakuomba wangu mwezi, sikiza kilio changu,
Toa nuru waziwazi, wala usiche mawingu,
Lisiwepo la tatizi, zing'arishe ndia zangu,
Nakuhitaji mwenzangu, kuishi peke siwezi.
Toa nuru waziwazi, wala usiche mawingu,
Lisiwepo la tatizi, zing'arishe ndia zangu,
Nakuhitaji mwenzangu, kuishi peke siwezi.
Ewe wangu mpumbazi, pumbaza karoho kangu,
Nikwambie laazizi, ni radhi nifunge pingu,
Nifunge pasi ajizi, gandalo ni haki yangu,
Nakuhitaji mwenzangu, kuishi peke siwezi.
Nikwambie laazizi, ni radhi nifunge pingu,
Nifunge pasi ajizi, gandalo ni haki yangu,
Nakuhitaji mwenzangu, kuishi peke siwezi.
Yeo juwa mkumbazi, penzi letu kama chungu,
Tumwombe Mola Mjuzi, atupatie mkungu,
Kufunika yetu kazi, wasiibe walimwengu,
Nakuhitaji mwenzangu, kuishi peke siwezi.
Tumwombe Mola Mjuzi, atupatie mkungu,
Kufunika yetu kazi, wasiibe walimwengu,
Nakuhitaji mwenzangu, kuishi peke siwezi.
Kaditama siongezi, hutoki moyoni mwangu,
Wafanyao mapinduzi, wafanye huko si kwangu,
Kupindua hawawezi, hii qadari ya Mungu,
Nakuhitaji mwenzangu, kuishi peke siwezi.
Wafanyao mapinduzi, wafanye huko si kwangu,
Kupindua hawawezi, hii qadari ya Mungu,
Nakuhitaji mwenzangu, kuishi peke siwezi.
22 Aprili 2017 Jumamosi 14:34
NjanoTano
Dotto Rangimoto Chamchuwa
Call/whatspp 0622845394 Morogoro.
NjanoTano
Dotto Rangimoto Chamchuwa
Call/whatspp 0622845394 Morogoro.
Comments
Post a Comment